Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 23

Ukombozi: Isa Al-Masihi anawafufua wafu

Surat Yohana 11:1-44

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake. 2 Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana Isa mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake. 3 Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Isa kumwambia, “Bwana Isa, yule umpendaye ni mgonjwa.”

4 Lakini Isa aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu [wa kiroho, si kimwili] apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” 5 Pamoja na hivyo, ingawa Isa aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao, 6 baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.

7 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.” 8 Wanafunzi wake wakamwambia, “Mwalimu, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”

9 Isa akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. 10 Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”

11 Baada ya kusema haya, Isa akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.” 12 Wanafunzi wakamwambia, “Bwana Isa, kama amelala usingizi ataamka.” 13 Hata hivyo, Isa alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.

14 Kwa hiyo Isa akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. 15 Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.” 16Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”

17 Isa alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. 18 Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili [yaani kama kilomita 3] , 19 nao Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. 20 Martha aliposikia kwamba Isa anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.

21 Martha akamwambia Isa, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. 22 Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”

23 Isa akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”

24 Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”

25 Isa akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

27 Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Al-Masihi, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

28 Baada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.” 29 Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Isa. 30 Isa alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha. 31 Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.

32 Maria alipofika mahali pale Isa alipokuwa, alipiga magoti miguuni pake na kusema, “Bwana Isa, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.” 33 Isa alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Isa alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34 Akauliza, “Mmemweka wapi?”

Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.” 35 Isa akalia machozi. 36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!” 37 Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”

38 Isa kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake. 39 Isa akasema, “Liondoeni hilo jiwe.”

Martha, ndugu yake yule aliyekuwa amekufa, akasema, “Lakini Bwana Isa, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.” 40 Isa akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”

41 Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Isa akainua macho yake juu, akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42 Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.” 43 Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti yake, akaita, “Lazaro, njoo huku!”

44 Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Isa akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2023 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.