Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 26

Ukombozi: Isa Al-Masihi anasalitiwa na kuhukumiwa

Surat Yohana 18:1-14; 19-24, 28-40; 20:1-16

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

18 Isa alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo. 2 Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Isa alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. 3 Hivyo Yuda akaja bustanini. Aliongoza kikosi cha askari wa Kirumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo.

Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha. 4 Isa akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”

5 Wao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri [yaani Isa alikuwa mtu kutoka Nasiri].”

Isa akawajibu, “Mimi ndiye.”

Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. 6 Isa alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini! 7Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.” 8 Isa akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.”

9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”

10 Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko. 11 Isa akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba [yaani ya kiroho, si kimwili]?”

12 Hivyo wale askari, wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Isa na kumfunga. 13 Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule [yaani kiongozi mkuu wa ibada]. 14 Kayafa ndiye alikuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.

19 Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Isa kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake. 20 Isa akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni [yaani nyumba za ibada], mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. 21 Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.”

22 Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Isa kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?” 23 Isa akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?”

24 Ndipo Anasi akampeleka Isa kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.

28 Ndipo Wayahudi wakamchukua Isa kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka.

29 Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”

30 Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”

31 Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”

Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.”

32 Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Isa kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.

33 Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Isa, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

34 Isa akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”

35 Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”

36 Isa akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”

37 Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?”

Isa akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”

38 Pilato akamuuliza Isa, “Kweli ni nini?”

Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Isa, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu. 39 Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”

40 Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyangʼanyi.

Ndipo Pilato akamtoa Isa akaamuru apigwe mijeledi. 2Askari wakasokota taji ya miiba, wakamvika Isa kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau. 3 Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu! Mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.

4 Pilato akatoka tena nje akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Isa kwenu kuwajulisha kwamba mimi sikumwona ana hatia.”

5 Kwa hiyo Isa akatoka nje akiwa amevaa ile taji ya miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, huyu hapa huyo mtu!”

6 Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”

Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe, mimi sioni hatia juu yake.”

7 Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”

8 Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi. 9Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Isa, “Wewe umetoka wapi?”

Lakini Isa hakumjibu. 10 Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”

11 Ndipo Isa akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”

12 Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Isa, lakini Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari [yaani mfalme mkuu]. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”

13 Pilato aliposikia maneno haya akamtoa Isa nje tena akaketi katika kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe (kwa Kiebrania paliitwa Gabatha).

14 Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”

15 Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”

Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”

Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”

16 Ndipo Pilato akamkabidhi Isa kwao ili wamsulubishe. Kwa hiyo askari wakamchukua Isa.

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.