Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 4

Anguko la wanadamu: Nuhu na Gharika Kuu

Surat Mwanzo 6:5-22; 7:1,10-11,17-20,23-24; 8:1,13,15-17,20-22; 9:1-17

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA TAURATI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

5 Bwana Mwenyezi Mungu akaona jinsi uovu wa mwanadamu ulivyokuwa mkubwa duniani, na ya kuwa kila mwelekeo wa mawazo ya moyo wake wakati wote ulikuwa mbaya tu.

6 Bwana Mwenyezi Mungu akasikitika kwamba alimuumba mwanadamu duniani, moyo wa Mungu ukajaa masikitiko. 7 Kwa hiyo Bwana Mwenyezi Mungu akasema, “Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba kutoka kwenye uso wa dunia, wanadamu na wanyama, pamoja na viumbe vitambaavyo na ndege wa angani. Kwa maana nasikitika kuwaumba.”

8 Lakini Nuhu akapata kibali machoni pa Bwana Mwenyezi Mungu.

9 Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, na mkamilifu miongoni mwa watu wa wakati wake, tena alitembea na Mungu. 10 Nuhu alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi. 11 Wakati huu dunia ilikuwa imejaa uharibifu na ukatili machoni pa Mungu. 12 Mungu akaona jinsi dunia ilivyoharibika, kwa maana watu wote duniani walikuwa wameharibu njia zao.

13 Kwa hiyo Mungu akamwambia Nuhu, “Nitawaangamiza watu wote, kwa kuwa dunia imejaa ukatili kwa sababu yao. Hakika mimi nitaangamiza watu pamoja na dunia.

14 Kwa hiyo jitengenezee safina kubwa kwa mbao za mvinje, tengeneza vyumba ndani yake na uipake lami ndani na nje. 15 Hivi ndivyo utakavyoitengeneza: Safina iwe na urefu wa dhiraa 300, upana wake dhiraa hamsini na kimo chake dhiraa thelathini [yaani safina ina urefu mita 135, upana mita 22 na nusu, na kimo mita 13 na nusu]. 16 Itengenezee paa na umalizie safina kwa kuacha nafasi ya dhiraa moja juu [yaani kama nusu mita]. Weka mlango ubavuni mwa safina, na uifanye ya ghorofa ya chini, ya kati na ya juu.

17 Nitaleta gharika ya maji juu ya nchi ili kuangamiza uhai wote chini ya mbingu, kila kiumbe chenye pumzi ya uhai ndani yake. Kila kitu juu ya nchi kitaangamia. 18 Lakini Mimi nitaweka Agano langu na wewe, nawe utaingia ndani ya Safina, wewe pamoja na mke wako, wanao na wake zao. 19 Utaingiza ndani ya Safina kila aina ya kiumbe hai wawili wawili, wa kiume na wa kike, ili kuwahifadhi hai pamoja na wewe.

20 Wawili wa kila aina ya ndege, wa kila aina ya mnyama na wa kila aina ya kitambaacho ardhini watakuja kwako ili wahifadhiwe hai. 21 Utachukua kila aina ya chakula kitakacholiwa, na ukiweke akiba kama chakula kwa ajili yako na yao.”

22 Nuhu akafanya kila kitu kama vile Mungu alivyomwamuru.

7 Ndipo Bwana Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki.

10 Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia. 11 Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili mwaka wa 600 wa kuishi kwake Nuhu, siku hiyo ndipo chemchemi zote hata zilizo chini sana ya ardhi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa.

17 Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani na maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka kwenye uso wa nchi. 18 Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya nchi, na safina ikaelea juu ya uso wa maji. 19 Maji yakazidi kujaa juu ya nchi, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote. 20 Maji yakaendelea kujaa yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano [yaani sawa na mita 7].

23 Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali, watu, wanyama, viumbe vitambaavyo na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Nuhu peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina. 24 Maji yakaifunika dunia kwa siku 150.

8 Mungu akamkumbuka Nuhu na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa naye ndani ya safina, akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakaondoka. 13 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 15 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu, 16 “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao. 17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”

20 Kisha Nuhu akamjengea Bwana Mwenyezi Mungu madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21 Bwana Mwenyezi Mungu akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya. 22 “Kwa muda dunia idumupo, wakati wa kupanda na wa kuvuna, wakati wa baridi na wa joto, wakati wa kiangazi na wa masika, usiku na mchana kamwe havitakoma.”

9 Ndipo Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akiwaambia, “Zaeni mkaongezeke kwa idadi na mkaijaze tena dunia. 2 Wanyama wote wa duniani, ndege wote wa angani, kila kiumbe kitambaacho juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu. 4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu ya uhai wake, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa mtu mwenzake. 6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu, damu yake itamwagwa na mwanadamu, kwa kuwa katika mfano wa Mungu, Mungu alimuumba mwanadamu.

7 Kuhusu ninyi, zaeni mwongezeke kwa wingi, mzidi katika dunia na kuijaza.” 8 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye: 9 “Sasa mimi ninaweka Agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10 pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: Ndege, wanyama wa kufugwa na wanyama wote wa porini, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi, kila kiumbe hai duniani. 11 Ninaweka Agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika, kamwe haitakuwepo tena gharika ya kuangamiza dunia.” 12 Mungu akasema, “Hii ni ishara ya Agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, Agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13 Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya Agano nifanyalo kati yangu na dunia.

14 Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukijitokeza mawinguni, 15 nitakumbuka Agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16 Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka Agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.” 17 Hivyo Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ndiyo ishara ya Agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2023 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.