Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 12

Ukombozi: Miujiza ya kuzaliwa kwa Isa Al-Masihi

Surat Luka 1:26-38; 2:1-20

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

26 Mwezi wa sita baada ya Elizabeti kupata mimba, Mwenyezi Mungu alimtuma malaika Jibraili aende Galilaya katika mji wa Nasiri, 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu mmoja jina lake Yusufu wa nyumba ya Daudi. Jina la huyu mwanamwali bikira ni Mariamu.

28 Naye malaika akaja kwake akamwambia: “Salamu, wewe uliyebarikiwa. Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe!”

29 Mariamu akafadhaishwa sana na maneno haya, akajiuliza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?”

30 Ndipo malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu, umepata kibali kwa Mwenyezi Mungu. 31 Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanaume na utamwita jina lake Isa. 32 Yeye atakuwa mkuu, naye ataitwa Mwana wa Aliye Juu Sana. Bwana Mwenyezi Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi baba yake. 33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho.”

34 Mariamu akamuuliza huyo malaika, “Maadamu mimi ni bikira, jambo hili litawezekanaje?”

35 Malaika akamjibu, “Roho wa Mwenyezi Mungu atakujilia juu yako, nazo nguvu zake Yeye Aliye Juu Sana zitakufunika kama kivuli. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mtakatifu, naye ataitwa Mwana wa Mungu [yaani Mwana wa kiroho, na sio kimwili]. 36 Tazama, jamaa yako Elizabeti amechukua mimba katika uzee wake, na huu ni mwezi wake wa sita, yeye aliyeitwa tasa. 37 Kwa maana kwa Mwenyezi Mungu hakuna lisilowezekana.”

38 Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mtumishi wa Mwenyezi Mungu. Na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka, akamwacha.

2 Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Kirumi. 2 Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Shamu. 3 Kila mtu alikwenda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.

4 Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nasiri ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. 5 Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, ambaye alikuwa amemposa, naye alikuwa mjamzito [Yusufu hakuwa baba mzazi wa Isa, bali alikuwa baba mlezi].

6 Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia, 7 naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.

8 Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9 Ghafula tazama, malaika wa Mwenyezi Mungu akawatokea, nao utukufu wa Bwana Mwenyezi ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu.

10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Al-Masihi Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”

13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, 14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”

15 Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Mwenyezi Mungu ametuambia habari zake.” 16 Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe.

17 Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. 18 Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. 19 Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. 20 Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.