Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 13

Ukombozi: Ushuhuda wa Yahya kuhusu Isa Al-Masihi

Surat Mathayo 3, Yohana 1:29-34

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

3 Siku hizo Yahya alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, 2 “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” 3 Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema: “Sauti ya mtu aliaye huko nyikani, ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, yanyoosheni mapito yake.’”

4 Basi Yahya alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 5 Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani.

6 Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani. [Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.] 7 Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi [hawa walikuwa aina ya wataalamu wa sheria] wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9 Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Ibrahimu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto kutoka kwa mawe haya. 10 Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

11 “Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho wa Mwenyezi Mungu na kwa moto. 12 Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”

13 Kisha Isa akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yahya ambatize. 14 Lakini Yahya akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?” 15 Lakini Isa akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yahya akakubali.

16 Naye Isa alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mwenyezi Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. 17 Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

29 Siku iliyofuata, Yahya alimwona Isa akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30 Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ 31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”

32 Kisha Yahya akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho wa Mwenyezi Mungu.’ 34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu [yaani Mwana wa kiroho, na sio kimwili].

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.