Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 17

Ukombozi: Isa Al-Masihi analisha watu elfu tano

Surat Yohana 6:1-37

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

6 Baada ya haya, Isa alikwenda ngʼambo ya Bahari ya Galilaya, ambayo pia huitwa Bahari ya Tiberia. 2 Umati mkubwa wa watu uliendelea kumfuata, kwa sababu waliona ishara nyingi za miujiza alizofanya kwa wagonjwa.

3 Kisha Isa akapanda mlimani akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. 4 Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia [yaani sherehe ya ukumbusho kutoka Misri kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu]. 5 Isa alipotazama na kuuona ule umati mkubwa wa watu ukimjia, akamwambia Filipo, “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” 6 Aliuliza swali hili kumpima, kwa maana alishajua la kufanya.

7 Filipo akamjibu, “Hata fedha kiasi cha dinari mia mbili [yaani ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 200], hazitoshi kununua mikate ya kuwapa watu hawa ili kila mtu apate kidogo.” 8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu yake Simoni Petro, akamwambia, 9 “Hapa kuna mvulana mmoja mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Lakini hivi vitatosha nini kwa umati huu wote?”

10 Isa akasema, “Waketisheni watu chini.” Palikuwa na majani mengi katika eneo lile, nao watu wakaketi. Palikuwa na wanaume wapatao 5,000. 11 Ndipo Isa akachukua ile mikate, akamshukuru Mungu na kuwagawia wale watu waliokuwa wameketi. Akafanya vivyo hivyo na wale samaki. Kila mtu akapata kadiri alivyotaka.

12 Watu wote walipokwisha kula na kushiba, akawaambia wanafunzi wake, “Kusanyeni vipande vilivyobaki vya ile mikate, kisipotee chochote.” 13 Hivyo wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili kwa vipande vya ile mikate mitano ya shayiri na samaki wale wawili wadogo vilivyobakishwa na waliokula.

14 Baada ya watu kuona muujiza ule Isa aliofanya, walianza kusema, “Hakika huyu ndiye Nabii ajaye ulimwenguni!” 15 Isa akijua kwamba walitaka kuja kumfanya awe mfalme wao, kwa nguvu, akajitenga nao akaenda milimani peke yake.

16 Ilipofika jioni, wanafunzi wake waliteremka kwenda baharini. 17 Wakaingia kwenye mashua, wakaanza kuvuka bahari kwenda Kapernaumu.

Wakati huu kulikuwa tayari giza na Isa alikuwa hajajumuika nao. 18 Bahari ikachafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda mwendo wa karibu maili tatu au nne [kama kilomita 5 au 6], walimwona Isa akitembea juu ya maji akikaribia mashua, nao wakaogopa sana.

20 Lakini Isa akawaambia, “Ni mimi. Msiogope.” 21 Ndipo wakamkaribisha kwa furaha ndani ya mashua, na mara wakafika ufuoni walikokuwa wakienda.

22 Siku iliyofuata, wale watu waliokuwa wamebaki ngʼambo waliona kwamba palikuwepo na mashua moja tu na kwamba Isa hakuwa ameondoka pamoja na wanafunzi wake, ila walikuwa wameondoka peke yao. 23 Lakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia zikafika karibu na mahali pale walipokula mikate baada ya Bwana Isa kumshukuru Mwenyezi Mungu.

24 Mara wale watu wakatambua kwamba Isa hakuwepo hapo, wala wanafunzi wake. Wakaingia kwenye mashua hizo, wakaenda Kapernaumu ili kumtafuta Isa.

25 Walipomkuta Isa ngʼambo ya bahari wakamuuliza, “Mwalimu, umefika lini huku?” 26 Isa akawajibu, “Amin, amin nawaambia, ninyi hamnitafuti kwa kuwa mliona ishara na miujiza, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msishughulikie chakula kiharibikacho, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele, ambacho Mwana wa Adamu atawapa. Yeye ndiye ambaye Mungu Baba Mwenyezi amemtia muhuri.”

28 Ndipo wakamuuliza, “Tufanye nini ili tupate kuitenda kazi ya Mungu?”

29 Isa akawajibu, “Kazi ya Mungu ndiyo hii: Mwaminini yeye aliyetumwa naye.”

30 Hivyo wakamuuliza, “Utafanya ishara gani ya muujiza, ili tuione tukuamini? Utafanya jambo gani? 31 Baba zetu walikula mana jangwani, kama ilivyoandikwa, ‘Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.’ ”

32 Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, si Musa aliyewapa mikate kutoka mbinguni, bali Baba yangu [wa kiroho, si kimwili] ndiye anawapa mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”

34 Wakamwambia, “Bwana Isa, kuanzia sasa tupatie huo mkate siku zote.”

35 Isa akawaambia, “Mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu, hataona njaa kamwe na yeye aniaminiye, hataona kiu kamwe. 36 Lakini kama nilivyowaambia, mmeniona lakini bado hamwamini. 37 Wale wote anipao Baba watakuja kwangu na yeyote ajaye kwangu, sitamfukuzia nje kamwe.

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.