Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 16

Ukombozi: Isa Al-Masihi amponya mtu mwenye pepo

Surat Marko 5:1-20

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

5 Wakafika upande wa pili wa ziwa wakaingia katika nchi ya Wagerasi. 2 Isa alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. 3 Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo. 4 Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5 Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

6 Alipomwona Isa kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake. 7 Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Isa, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8 Kwa kuwa Isa alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”

9 Isa akamuuliza, “Jina lako ni nani?” Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tuko wengi.” 10 Akamsihi Isa sana asiwapeleke nje ya nchi ile.

11 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima. 12 Wale pepo wachafu wakamsihi Isa wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.”

13 Basi Isa akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.

14 Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia.

15 Walipofika kwa Isa, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu legioni akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa. 16 Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia. 17 Basi watu wakaanza kumwomba Isa aondoke katika nchi yao.

18 Isa alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Isa waende pamoja. 19 Isa hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyokuhurumia.” 20 Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli [yaani miji kumi katika nchi ya Wagerasi] mambo makuu Isa aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2023 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.