Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 19

Ukombozi: Isa azungumza na mwanamke msamaria

Surat Yohana 4:1-26, 39-42

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

4 Mafarisayo wakasikia kwamba Isa alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yahya, [*Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.] 2 ingawa kwa kweli si Isa mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. 3 Bwana Isa alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya. 4Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. 5Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu.

6 Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana. 7 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.” 8Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula. 9

Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.

10 Isa akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”

11 Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”

13 Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki, ataona kiu tena. 14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.”

15Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”

16 Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.” 17Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”

Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. 18 Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”

19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. 20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”

21 Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba [yaani Mwenyezi Mungu] katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Al-Masihi) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.” 26 Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”

39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” 40 Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. 41 Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.

42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.”

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.