
Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.
KUTOKA INJILI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI
Mfano Wa Msamaria Mwema
25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa sheria alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Isa akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”
27 Akajibu, “ ‘Mpende Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’”
28 Isa akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”
29 Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionyesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, “Jirani yangu ni nani?”
30 Isa akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyangʼanyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja [yaani kiongozi wa dini] alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja [yaani mfanyakazi kwenye nyumba ya ibada] naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani.
33 Lakini Msamaria mmoja [Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria] aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni na kumtunza.
35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili [yaani sawa na mshahara wa kibarua kwa siku mbili] akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’ 36
“Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyangʼanyi?”
37 Yule mtaalamu wa Torati akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”
Ndipo Isa akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
Mfano Wa Mwana Mpotevu
11 Isa akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12 Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.
13 “Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokuwa navyo, akaenda nchi ya mbali, na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. 14 Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana chochote. 15 Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa chochote.
17 “Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! 18 Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. 19Sistahili tena kuitwa mwanao; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’ 20 Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. 21 “Yule mwana akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’
22 “Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, tieni pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake. 23 Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. 24 Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena; alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija.
25 Wakati huo, yule mwana mkubwa alikuwa shambani. Alipokaribia nyumbani, akasikia sauti ya nyimbo na watu wakicheza. 26 Akamwita mmoja wa watumishi na kumuuliza, ‘Kuna nini?’ 27 Akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, naye baba yako amemchinjia ndama aliyenona kwa sababu mwanawe amerudi nyumbani akiwa salama na mzima.’
28 “Yule mwana mkubwa akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi baba yake akatoka nje na kumsihi. 29Lakini yeye akamjibu baba yake, ‘Tazama! Miaka yote hii nimekutumikia na hata siku moja sijaacha kutii amri zako, lakini hujanipa hata mwana-mbuzi ili nifurahi na rafiki zangu. 30 Lakini huyu mwanao ambaye ametapanya mali yako kwa makahaba aliporudi nyumbani, wewe umemchinjia ndama aliyenona!’
31 “Baba yake akamjibu, ‘Mwanangu, umekuwa nami siku zote na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32 Lakini ilitubidi tufurahi na kushangilia kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa na sasa yu hai; alikuwa amepotea naye amepatikana.’”
Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.
Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.
Get Discovery Bible Studies on your phone
Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org
Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.