
Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.
Wakati Ibrahimu anamsubiri Mwenyezi Mungu amtimizie ahadi yake kumpa mtoto na mkewe Sara, akamzaa Ismael akiwa pamoja na Hajra, mtumishi wa mke wake. Baadaye Mwenyezi Mungu amewapa Ibrahimu na mkewe Sara Isaka, ambaye ni mtoto wao wa pekee.
KUTOKA TAURATI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI
22 Baadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!” Ibrahimu akajibu, “Mimi hapa.”
2 Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaka umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
3 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali.
5 Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”
6 Ibrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7 Isaka akanena akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!” Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”
Isaka akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?” 8 Ibrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.”
Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja. 9 Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.
11 Lakini malaika wa Bwana Mwenyezi Mungu akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!” Akajibu, “Mimi hapa.” 12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13 Ibrahimu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
14 Ibrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire [maana yake Mwenyezi Mungu atatupa]. Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima wa Bwana Mwenyezi Mungu itapatikana.”
15 Basi malaika wa Bwana Mweyenzi Mungu akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana Mwenyezi Mungu, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani.
Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19 Ndipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer- Sheba. Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.
Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.
Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.
Get Discovery Bible Studies on your phone
Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org
Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.