
Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.
KUTOKA TAURATI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI
6 “Kwa hiyo, waambie Waisraeli: ‘Mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu, nami nitawatoa mtoke katika kongwa la Wamisri. Nitawaweka huru mtoke kuwa watumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa pamoja na matendo makuu ya hukumu.
7 Nitawatwaa mwe watu wangu mwenyewe, nami nitakuwa Mungu wenu. Ndipo mtajua kuwa mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu wenu, niliyewatoa chini ya kongwa la Wamisri. 8 Nami nitawaleta mpaka nchi niliyoapa kwa mkono ulioinuliwa kumpa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Nitawapa iwe milki yenu. Mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu.’ ”
12 Bwana Mwenyezi Mungu akamwambia Musa na Haruni katika nchi ya Misri, 2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu, yaani mwezi wa kwanza wa mwaka wenu. 3 Iambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba.
5 Wanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. 6 Tunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni.
7 Ndipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. 8 Usiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu [yaani hamira].
11 Hivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Bwana Mwenyezi Mungu.
12 “Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu.
13 Damu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.
14 “Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu, mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa Bwana Mwenyezi Mungu, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu.
21 Ndipo Musa akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.
22 Chukueni kitawi cha hisopo [aina ya mmea], kichovyeni kwenye damu iliyopo kwenye sinia na kuipaka baadhi ya hiyo damu kwenye vizingiti na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake mpaka asubuhi. 23 Bwana Mwenyezi Mungu apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.
24 “Shikeni maagizo haya yawe kanuni ya kudumu kwenu na kwa ajili ya wazao wenu. 25 Mtakapoingia katika nchi Bwana Mwenyezi Mungu atakayowapa kama alivyoahidi, shikeni desturi hii. 26 Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’
27 Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa Bwana Mwenyezi Mungu, ambaye alipita juu ya nyumba za Waisraeli katika nchi ya Misri na hakudhuru nyumba zetu alipowapiga Wamisri.’ ”
Ndipo watu wa Israeli waliposujudu na kuabudu. 28 Waisraeli wakafanya kama vile Bwana Mwenyezi Mungu alivyomwagiza Musa na Haruni.
29 Ilipofika usiku wa manane, Bwana Mwenyezi Mungu akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, kuanzia mzaliwa wa kwanza wa Farao, mrithi wa kiti cha ufalme, hadi mzaliwa wa kwanza wa mfungwa, aliyekuwa gerezani, na wazaliwa wa kwanza wa mifugo yote pia. 30 Farao, na maafisa wake wote, na Wamisri wote wakaamka usiku, na kulikuwa na kilio kikubwa katika nchi ya Misri, kwa kuwa haikuwepo nyumba ambayo hakufa mtu.
31 Wakati huo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, “Ondokeni! Tokeni kwa watu wangu, ninyi pamoja na Waisraeli! Nendeni mkamwabudu Bwana Mwenyezi Mungu kama mlivyoomba.
Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.
Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.
Get Discovery Bible Studies on your phone
Discover copyright ©2015-2026 discoverapp.org
Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.