Gundua Vitabu Vitakatifu

Somo la 9

Ukombozi: Sheria kuhusu sadaka ya dhambi

Surat Malawi 4:1-2,13-31

Isome nakala

Soma au sikiliza nakala inayofuata. Soma au sikiliza tena nakala hii mpaka utakapoifahamu vizuri.

x1.0

KUTOKA TAURATI, TAFSIRI KWA LUGHA NA MILA ZA WASWAHILI

4 Bwana Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2 “Waambie Waisraeli: ‘Mtu yeyote afanyapo dhambi bila kukusudia na akatenda lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mwenyezi Mungu: “

13 “ ‘Ikiwa jumuiya yote ya Israeli watatenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mwenyezi Mungu hata kama jumuiya haifahamu juu ya jambo hilo, wana hatia. 14 Wanapotambua kuhusu dhambi waliyoitenda, lazima kusanyiko lilete fahali mchanga [kwa maana ya ng’ombe dume] kuwa sadaka ya dhambi na kuikabidhi mbele ya Hema la Kukutania.

15 Wazee wa jumuiya wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali aliye mbele za Bwana Mwenyezi Mungu, naye fahali atachinjwa mbele za Bwana Mwenyezi Mungu. 16 Kisha kuhani aliyetiwa mafuta [yaani kiongozi wa ibada] ataiingiza sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya Hema la Kukutania.

17 Atachovya kidole chake kwenye damu na kuinyunyiza mara saba mbele za Bwana Mwenyezi Mungu mbele ya hilo pazia. 18 Atatia sehemu ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu yaliyo mbele za Bwana Mwenyezi Mungu katika Hema la Kukutania. Damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu ya kuteketezea sadaka, penye ingilio la Hema la Kukutania.

19 Atayaondoa mafuta yote ya yule fahali na kuyateketeza juu ya madhabahu, 20 naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa.

21 Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya.

22 “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mwenyezi Mungu wake, ana hatia. 23 Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete mbuzi dume asiye na dosari kama sadaka yake. 24 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale ambapo sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za Bwana Mwenyezi Mungu. Hii ni sadaka ya dhambi.

25 Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. 26 Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa.

27 “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya Bwana Mwenyezi Mungu, yeye ana hatia.

28 Atakapofahamishwa dhambi yake aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kama sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda. 29 Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka.

30 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. 31 Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza Bwana Mwenyezi Mungu.

Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.

Simulia nakala hii kwa maneno yako

Tumia muda mfupi ukiisimulia tena simulizi kwa maneno yako mwenyewe. Unaweza kuisimulia kwa sauti au kuiandika. Ukiona unahangaika kuikumbuka, isome au uisikilize tena.

Igundue nakala

Ukiona umeielewa simulizi, uvute ilham. Tumia muda kuifikiria au jadili maswali yafuatayo. Ni vizuri kuyapitia masomo haya pamoja na familia na marafiki zako ili mpate kujifunza na kushirikiana kwa pamoja.


Get it on Google Play
Download on the App Store

Get Discovery Bible Studies on your phone

Discover copyright ©2015-2023 discoverapp.org

Swahili verses from the Kiswahili Contemporary Scriptures (Neno: Maandiko Matakatifu). Copyright © 2018 by Biblica, Inc.® All Rights Reserved Worldwide.